Psalms 39

Maombi Ya Mtu Anayeteseka

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Yeduthuni. Zaburi Ya Daudi)


1 aNilisema, “Nitaziangalia njia zangu
na kuuzuia ulimi wangu usije ukatenda dhambi;
nitaweka lijamu kinywani mwangu
wakati wote waovu wanapokuwa karibu nami.”

2 bLakini niliponyamaza kimya na kutulia,
hata pasipo kusema lolote jema,
uchungu wangu uliongezeka.

3 cMoyo wangu ulipata moto ndani yangu,
nilipotafakari, moto uliwaka,
ndipo nikasema kwa ulimi wangu:


4 d“Ee Bwana, nijulishe mwisho wa maisha yangu
na hesabu ya siku zangu;
nijalie kujua jinsi maisha yangu
yanavyopita upesi.

5 eUmefanya maisha yangu mafupi kama pumzi;
muda wangu wa kuishi ni kama
hauna thamani kwako.
Maisha ya kila mwanadamu
ni kama pumzi.

6 fHakika kila binadamu ni kama njozi
aendapo huku na huko:
hujishughulisha na mengi lakini ni ubatili;
anakusanya mali nyingi,
wala hajui ni nani atakayeifaidi.


7 g“Lakini sasa Bwana, nitafute nini?
Tumaini langu ni kwako.

8 hNiokoe kutoka kwenye makosa yangu yote,
usinifanye kuwa dhihaka ya wapumbavu.

9 iNilinyamaza kimya,
sikufumbua kinywa changu,
kwa sababu wewe ndiwe uliyetenda hili.

10 jNiondolee mjeledi wako,
nimeshindwa kwa mapigo ya mkono wako.

11 kUnakemea na kuadhibu wanadamu
kwa ajili ya dhambi zao;
unaharibu utajiri wao kama nondo aharibuvyo:
kila mwanadamu ni kama pumzi tu.


12 l“Ee Bwana, usikie maombi yangu,
usikie kilio changu unisaidie,
usiwe kiziwi kwa kulia kwangu.
Kwani mimi ninaishi na wewe kama mgeni,
kama walivyokuwa baba zangu wote,

13 mTazama mbali nami, ili niweze kufurahi tena
kabla sijaondoka na nisiwepo tena.”
Copyright information for SwhKC